Abstract:
Mawasiliano ni suala la msingi katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Ni mojawapo ya nyenzo anazotumia mwanadamu kwa lengo la kupasha habari kwa walengwa wake. Anaweza akaonyesha hisia za furaha, huzuni, mapenzi au hata matumaini yake. Miongoni mwa jamii za Wapwani, mawasiliano haya hufanikishwa kwa namna kadha wa kadha zikiwemo nyimbo za taarab. Kwa hivyo, utafiti huu ulilenga kufumbua maana kusudiwa katika sitiari za taarab za watribu teule kama chombo cha mawasiliano kwa kusimba maana miongoni mwa jamii za Pwani, Unguja. Utafiti huu ulikuwa na madhumuni matatu; kutambua sitiari katika taarab za Mzee Yusuf na Mwanahawa Ally, kubainisha dhima kimawasiliano za sitiari katika nyimbo za taarab za Mzee Yusuf na Mwanahawa Ally na kuonyesha sababu zinazowafanya watribu hawa kusimba maana katika utunzi wa taarab kwa kutumia kauli zao kisitiari. Ili kutekeleza haya, nadharia ya Uhusiano ilikuwa nguzo kuu pamoja na nadharia ya dhana-sitiari. Utafiti huu ulihusisha muundo wa uchanganuzi kifani. Sampuli ya kimakusudi ilitumiwa kuteua nyimbo mbili mbili za taarab kutoka kwa watribu wawili teule kutoka Unguja. Data ilikusanywa kupitia usomaji matini kwa kusoma makala kuhusu nyimbo za taarab na kusikiliza na kutazama kanda zenye nyimbo teule za taarab na kunakili kauli na maelezo mwafaka kutokana na nyimbo hizo. Data zilizopatikana zilichambuliwa kwa misingi ya nadharia teule katika utafiti huu kwa kutumia uchanganuzi-fafanuzi. Kutokana na uchanganuzi wetu, matokeo yalionyesha kuwa watribu wa nyimbo za taarab kutoka Zanzibar huwasilisha ujumbe wao kisitiari. Vilevile, ilibainika kwamba katika ufumbaji huo, nyimbo hizi hutekeleza majukumu kadha yakiwemo kumulika mahusiano na changamoto zinazowakumba wanajamii. Zaidi ya hayo, iligunduliwa kuwa maana kusudiwa katika nyimbo hizi inaweza kuelezewa kwa misingi ya kiuamali. Utafiti huu utakuwa na manufaa kwa kuwa mawasiliano kwa njia ya kusimba maana yataimarishwa miongoni mwa jamii kwa sababu kadha ikiwemo kuendeleza tasfida na kukuza maadili miongoni mwa wanajamii. Matokeo ya utafiti huu yatawanufaisha watribu kwa kuwaongoza katika uteuzi mwafaka wa kauli kutegemea muktadha wa utunzi, wasikilizaji watapata mwongozo wa kutambua kwa urahisi maana kusudiwa na watribu na wasomi wa fasihi na isimu kwa kupata mwanga wa kuendeleza tafiti zinahusiana na utafiti huu wakiongozwa na nadharia teule katika uchanganuzi huu.