Abstract:
Utafiti huu ulilenga kuchanganua matumizi ya agoti miongoni mwa wafungwa wa magereza ya Kisumu. Utafiti huu utachangia tafiti katika taasisi na vyuo vikuu kwa sababu uliibua muktadha wa matumizi ya lugha ambao haujatafitiwa nchini Kenya. Utafiti huu ulikuwa na madhumuni matatu; kujadili vikoa maana katika agoti zinazotumiwa na wafungwa wa magereza ya Kisumu. Pili, kufafanua mabadiliko ya kimaana yanayojitokeza katika agoti zinazotumiwa na wafungwa wa magereza ya Kisumu. Tatu, kujadili mbinu za uundaji wa agoti zinazotumiwa na wafungwa wa magereza ya Kisumu. Mtafiti alijikita katika Nadharia ya Pragmatiki Leksika ambayo huchunguza jinsi maana ya neno kiisimu hubadilika kimatumizi. Utafiti huu uliongozwa na muundo wa usoroveya elezi. Kupitia kwayo mtafiti alifanikiwa kupata habari alizotaka kuhusu agoti za wafungwa. Data ilikusanywa kwa kutumia kalamu na daftari. Utafiti wenyewe ulifanywa katika magereza ya Kibos na Kodiaga mjini Kisumu. Uteuzi wa sampuli kusudio ulitumiwa kupata watafitiwa mia moja themanini na watano ambao walishirikishwa katika utafiti. Jumla ya agoti mia mbili sitini na tatu zilikusanywa na kutokana na idadi hii, mtafiti aliteua agoti mia moja themanini na nane ambazo zilichanganuliwa. Agoti hizi ndizo zilizotimiza upeo na mipaka ya utafiti huu. Usaili na mahojiano ya kimakundi yalitumiwa kama mbinu za kukusanya data. Data ilichambuliwa kwa misingi ya nadharia iliyoteuliwa na kwa kutumia mkabala wa kimaelezo. Utafiti huu ulifanikiwa kufafanua vikoa vitano vya maana ambavyo agoti za wafungwa huweza kuanishwa kwayvyo. Mtafiti alidhihirisha kuwa baadhi ya leksimu zenye maana kiisimu hubadili maana kimatumizi katika muktadha wa jela. Ubanaji na upanuzi wa maana ulijitokeza kama mabadiliko makuu ya kimaana katika agoti za wafungwa. Isitoshe, utafiti huu ulifanikiwa kujadili mbinu mbalimbali za uundaji wa agoti zinazotumiwa na wafungwa wa magereza ya Kisumu. Utafiti huu ulifikia hitimisho kuwa agoti za wafungwa ni hazina ya maana kutokana na jinsi wafungwa walivyoonyesha ubunifu wa kuyapa maneno maana, kubadili maana ya maneno na kwa kubuni leksimu za kuwasiliana miongoni mwao. Hatimaye utafiti huu ulitoa mapendekezo kwa watafiti wa baadaye ambao wangependa kushughulikia eneo la lugha ya wafungwa.