Abstract:
Katika uwasilishaji wa kazi yoyote ya kifasihi, lugha huwa kipengele cha umuhimu sana.
Utafiti huu ulinuia kuchunguza lugha ya kisitiari katika usawiri wa masuala ya kisiasa katika
riwaya ya Kiza katika Nuru na Chozi la Heri. Utafiti ulizingatia malengo yafuatayo:
Kudhihirisha matumizi ya lugha ya kisitiari ili kusawiri siasa katika Chozi la Heri na Kiza
katika Nuru, Kufafanua taashira zilizojengwa na lugha ya kisitiari katika Chozi la Heri na
Kiza katika Nuru, Kutathmini jinsi lugha ya kisitiari ilivyotumika katika kuwaumba
wahusika ili kuibua masuala ya kisiasa katika Kiza katika Nuru na Chozi la Heri. Utafiti
uliongozwa na nadharia ya umitindo iliyoasisiwa na Viktor Shklovsky mwaka wa 1904.
Kulingana na nadharia hii, mwandishi wa kazi za kifasihi hutumia lugha yenye maana fiche
huku akimuwezesha msomaji kuwa na mwelekeo mpya kuhusu kitu cha kawaida tu. Mhimili
mkuu wa nadharia ya umitindo ni kwamba maana katika kazi za fasihi huwasilishwa kwa
njia fiche. Mwandishi wa kazi za fasihi hutumia lugha ya kitamathali kama vile tashbihi,
taashira, methali, misemo miongoni mwa zingine ili kupata mtindo usio wa moja kwa moja.
Utafiti ulichukua muundo elezi. Katika usampulishaji, riwaya zilizoteuliwa ni pamoja na
Chozi la Heri na Kiza katika Nuru. Riwaya hizi ziliteuliwa kimaksudi kwa sababu baada ya
usomaji wa awali ilidhihirika kwamba lugha ya kisitiari katika kuibua masuala ya kisiasa
imejitokeza mno. Ukusanyaji wa data ulijumuisha kusoma riwaya teule na kudondoa
vipengele vya lugha ya kisitiari vilivyobeba masuala ya kisiasa. Aidha, kazi zingine
zilizokuwa na umuhimu katika utafiti huu zilirejelewa. Baada ya kukusanya data,
uchanganuzi na uhariri wa data hiyo uliendelezwa huku ukiongozwa na nadharia na malengo
ya utafiti. Utafiti ulibaini kuwa waandishi wa riwaya ya Kiza katika Nuru na Chozi la Heri
wametumia lugha ya kisitiari sana kujenga masuala ya kisiasa. Waandishi wa riwaya hizi
wamefanikisha kazi zao kifani kupitia matumizi ya lugha ya kisitiari katika kujenga masuala
ya kisiasa. Masuala ya kisiasa yaliyojengwa na mbinu hizi ni pamoja na: upigaji kura, vita
vya baada ya uchaguzi, viongozi kutumia vijana kuendeleza mapigano, ufisadi, nafasi ya
mwanamke katika siasa/uongozi, dhuluma kwa raia, kuuliwa kwa wapinzani na watetezi wa
haki miongoni mwa mengine. Kitaalamu, matokeo ya utafiti huu yatawanufaisha wasomaji
na wahakiki wa riwaya ya Kiswahili katika kuelewa zaidi kuhusu jinsi lugha ya kisitiari
imetumika katika kujenga masuala ya kisiasa katika riwaya ya Kiswahili. Kinadharia, utafiti
huu utawafaa watafiti wengine watakaotumia nadharia ya umitindo katika kuchanganua kazi
zingine za kifasihi. Inapendekezwa kwamba watafiti wengine wanaweza kuchuguza
matumizi ya lugha ya kisitiari katika kuibua masuala mengine yasiyo ya kisiasa katika riwaya
ya Kiswahili.